Makala - Historia ya Hip Hop Tanzania
Bongo Flava ni jina badala la muziki
wa Hip hop ya Tanzania. Mtindo huu ulianzishwa kwenye miaka ya 1990, hasa ukiwa
kama mwigo au utokanaji wa hip hop kutoka Marekani, ikiwa na ongezeko la athira
ya muziki wa reggae, R&B, afrobeat, dancehall, na mitindo ya asili ya
Kitanzania kama vile taarab na dansi, muunganiko ambao umeunda mtindo wa pekee
wa muziki Mashairi kawaida huwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza.
Jina la
"bongo flava" ni tokeo la matini yaliyoharibiwa kutoka "bongo
flavour", ambapo "bongo" ni wingi wa neno ubongo ambapo mara nyingi huchukua
nafasi ya kutaja jina la utani la Dar es Salaam, jiji ambalo mtindo aina ya
mtindo huu inatokea. Katika bongo flava, sitiari ya "bongo" inaweza
kutaja zaidi maana ya ujanjaujanja wa mtaani, ya msela au masela wingi
wake.
Istilahi ya
"bongo flava" ilitajwa kwa mara ya kwanza mnamo 1996 na Radio One
99.6 FM (moja kati ya redio za kwanza kabisa za binafsi nchini Tanzania) DR wa
Redio Mike Mhagama ambaye alikuwa akijaribu kutofautisha kati ya muziki wa R
& B na hip hop wa Marekani kupitia lipindi chake maarufu cha redio - 'DJ
Show' ambapo enzi hizo vijana chipukizi walikuwa hawajaanza kutamba kwa mitindo
yao wenyewe. DJ Show kilikuwa kipindi cha kwanza cha redio kukubali wanamuziki
vijana wa Kitanzania wenye athira ya muziki wa Marekani - wakijieleza wenyewe
kupitia uimbaji wa rap. Alisema hewani, "Baada ya kusikiliza kibao cha
"R & B Flava" kilichoitwa 'No Diggity' kutoka Marekani, sasa
inakuja "Bongo Flava" kutoka kwa Unique Sisters, kutoka hapa
nyumbani." Baada ya kusema hivyo katika kipindi, istilahi hii ya
"Bongo Flava" ikanasa hadi leo hii.
Asili ya mwanzo
kabisa na jinsi "Bongo flava" ilivyoanzishwa nchini Tanzania ni
kutokana na Taji Liundi akiwa kama kiini cha hadithi hii. Kifupi hakuna asili
bila yeye. Taji Liundi pia anajulikana kama Master T, mwasisi, mwanzilishi na
vilevile mtayarishaji wa kipindi cha Dj Show alishaanza kupiga nyimbo za
wasanii wa ndani tangu mwishoni mwa miaka ya 1994. Mike Mhagama baadaye
akajiunga na kipindi akiwa chini ya ukufunzi wa Master T. Aliendelea na
kutangaza kipindi hicho peke yake hata baada ya Master T kuondoka Radio One
mnamo 1996.
"Bongo
flava" ilikaa vizuri sana hata kabla ya rekodi za video au sauti. Vijana
mjini Dar es salaam walikuwa wakirap ufukweni mwa bahari kupitia matamasha
mbalimbali (yameandaliwa na Joseph Kusaga ambaye anamiliki Mawingu Discothèque,
baadaye Mawingu Studios na sasa ni Clouds Media Group, matamasha ya ndani
yaliyochukua sura mpya rasmi baada ya kuanzisha mfululozo wa shindano la Yo!Rap
Bonanza ambalo lilikuwa likichochewa na DJ Kim "And the Boyz"
Magomelo.
Baadhi ya
vijana walikuwa wakijipanga au kujiita majina ya kutunga au kundi fulani,
baadhi yao walikuwa wakijitegemea au kujiweka katika kikundi fulani katika
tukio hilo ilimradi wapate nafasi ya kukamata mic. Moja kati ya waliowahi
kutamba katika mashindano ya kushika mic mwanzoni mwa miaka ya 1990 ni pamoja
na Adili au Nigga One. Msanii maarufu wa kwanza wa mtindo huu aliyewahi kuiga
ngoma za Marekani ni Saleh Jabir ambaye alirap kwa Kiswahili kupitia biti ya
Vanilla Ice, "Ice Ice Baby", yeye ndiye aliyeanza kuweka Kiswahili
katika rap. Toleo lake lilikuwa maarufu, ilivunja rekodi na kuweza kupigwa hata
katika Redio ya Taifa la Tanzania. Ulikuwa wimbo wa kwanza wa rap ya Kiswahili
kupaa anga ya Tanzania.
Moja kati ya
makundi ya mwanzo kabisa kurekodi na kupeleka CD Radio One ili irushwe ilikuwa
bendi ya Mawingu, kundi ambalo lilitamba sana mwanzoni mwa miaka ya 1994.
Walirekodia katika Studio za Mawingu. Wanachama wake walikuwa kina Othman Njaidi,
Eliudi Pemba, Columba Mwingira, Sindila Assey, Angela, Robert Chuwa, Boniface
Kilosa (a.k.a. Dj Boni Love) na baadaye Pamela ambaye aliimba kibao chao
kilichovunja rekodi cha RnB/Rap "Oya Msela". Wimbo ulikuwa maarufu
mno na baadaye hilo neno likabaki hadi leo. Bendi ya Mawingu hujadilika kama
waanzilishi wa ladha aina ya RnB ya Bongo flava. Dar Young Mob lilikuwa kundi
la kwanza la hip hop ya kweli kurekodi na Mawingu Studios chini ya utayarishaji
wake Dj Boni Love. Lilikuwa kundi la kwanza kupigiwa kibao chao katika redio ya
binafsi nchini Tanzania.
Mwanzilishi wa
hip hop ya Tanzania ni Mr. II (pia anajulikana kama Sugu au 2-Proud), ambaye
alitoa kibao chake cha kwanza maarufu cha Bongo flava, Ni Mimi mnamo
1995. Mr. II bado yupo hadi leo (rekodi yake ya mwisho ni Coming of Age, ilitolewa mnamo 2007).
Kundi la kwanza la hip hop la Tanzania, Kwanza Unit, 1993. Awali walikuwa
wanaimba kwa Kiingereza lakini hatimaye wakawa wanaimba kwa Kiswahili. Moja
kati ya wanachama wa zamani wa kundi hili ni Professor Jay, kwa ni moja kati ya
wasanii maarufu wa hip hop nchini Tanzania. Vilevile kundi la Diplomate
lililokuwa na kina Saigon.
Miongoni mwa
wasanii maarufu wa Bongo Flava kwa sasa ni pamoja na Ali Kiba, Juma Nature, Lady
Jaydee, Mzungu Kichaa, Geezy Mabovu, Q Chillah, TID, Diamond Platnumz, Dknob na
wasanii wapya wa Bongo Flava kama vile Nay wa Mitego, Ben Pol, Dogo Fani na
wengine wengi. Majina mengine maarufu ni pamoja na Gangwe Mobb, Dully Sykes, na
Daz Baba.
Comments
Post a Comment