MAKALA - USIYOYAJUA KUHUSU UGONJWA WA MATENDE
USIYOYAJUA KUHUSU
UGONJWA WA MATENDE
Ugonjwa wa matende ni aina ya ugonjwa unaosababisha ngozi na
tishu zilizo chini ya ngozi ya mwanadamu kuwa nene (thickening of skin and
underlying tissue).Ugonjwa huu huathiri miguu,mikono, figo, korodani na kusababisha
korodani kuvimba na kuwa kubwa sana.
Inakisiwa watu milioni 120 duniani wana maambukizi ya ugonjwa
huu ambapo kati yao milioni 40 wamepata madhara makubwa kutokana na ugonjwa huu.
Kati ya hawa walioathirika theluthi moja huapatikana katika
bara la Afrika, theluthi moja nyingine hupatikana India,na kiwango kilichobakia
hupatikana katika visiwa vya Pacific, Marekani na Asia ya kusini.
Aina nyingine ya ugonjwa wa matende inayojulikana kama
nonparasitic elephantiasis au podoconiosis ambayo haisababishwi na vimelea
vyovyote hupatikana katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, Tanzania,
Rwanda,Burundi) Sudan, Egypt na Ethiopia.Asilimia 6 ya maambukizi ya aina hii
ya podoconiosis hupatikana nchini Ethiopia.
Nini hutokea baada ya
maambukizi?
Kwa kawaida mtu
aliyeambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu (larvae) kwenye mfumo wa damu mwilini
mwake wanaojulikana kama microfilariae. Mabuu haya husafiri kutoka kwenye mfumo
wa damu hadi kwenye mfumo mwingine unaojulikana kama mfumo wa limfu (lymphatic system)
na kukua kuwa minyoo kamili (adult worms) ambayo huziba mfumo huu wa limfu
ambao unategemewa sana katika kuweka uwiano sawa wa maji (fluid balance) kati
ya mfumo wa damu na tishu ndani ya mwili na husaidia kuupa mwili kinga dhidhi
ya magonjwa mbalimbali. Minyoo hii huishi kwa miaka minne hadi sita na katika
uhai wake huzaa mamilioni ya mabuu (microfilariae) mengine wakati ikiwa kwenye
mfumo wa damu.
Mbu huenezaje ugonjwa
huu?
Mtu ambaye
ameambukizwa ugonjwa huu huwa na mabuu kwenye mfumo wake wa damu na anapongatwa
na mbu ambawo wanauwezo wa kuchukua mabuu haya ambayo huendelea kukua na
kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine ndani ya mwili wa mbu.
Kwa kawaida, ukuaji huu wa mabuu ndani ya mwili wa mbu huchukua
wiki moja hadi tatu na baada ya kukua na kufikia hatua ya kuambukiza mtu mwingine,
mabuu haya husogea mpaka kwenye sehemu ya mdomo wa mbu ambayo ndio huwa
humng'ata mtu wakati mbu anapofyonza damu kutoka kwa mtu.
Mbu mweye mabuu kwenye mdomo wake anapomngata mtu ili
kufyonza damu, ndipo mabuu haya yanapoingia kwenye mwili wa mtu na hivyo
kusababisha maambukizi ya ugonjwa huu.
Dalili za ugonjwa huu
ni zipi?
• Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kuvimba sehemu ya chini ya
mwili yaani kwenye miguu na vidole.Pia mtu anaweza kuvimba sehemu ya mikono au
mkono wote pamoja na vidole vya mkononi. Wengine huvimba kwenye korodani
(wanaume).
• Kuhisi uzito na kukamaa kwa mikono au miguu kutokana na
uvimbe uliopo.
• Kutoweza kutumia kiungo husika kilichovimba.
• Maumivu au kutohisi vizuri kwenye mikono au miguu.
• Kupata maambukizi ya mara kwa mara kwenye sehemu
iliyovimba.
• Ngozi kuwa nene na ngumu kwenye mikono au miguu.
Dalili nyingine ni
pamoja na;
- Homa
- Maumivu ya kichwa
- Maumivu kwenye jointi na mifupa
- Kutapika
- Vidonda kwenye mikono au miguu
- Mistari ya rangi nyekundu inayoonekana kwenye mikono au
miguu (red streaks)
Vipimo vya uchunguzi
• Blood examination under microscope - Kipimo cha kuangalia
damu kwenye hadubini ili kuangalia kama kuna mabuu ya ugonjwa huu wa matende. Kwa
wale ambao wana ugonjwa huu kwa muda mrefu, mabuu hayaonekani kwenye damu kwani
tayari yatakuwa yameshaingia kwenye mfumo wa limfu. Hivyo, kutoonekana kwa
mabuu kwenye damu kwa kutumia hadubini si kigezo cha kusema kwamba mgonjwa hana
ugonjwa huu wa matende.
• Vipimo vyengine vinavyoweza kutumika ni pamoja na CT Scan,
MRI, Doppler Ultrasound, Radionuclide Imaging ili kuweza kutofautisha ugonjwa
huu na magonjwa mengine yanayosababisha kuvimba kwa miguu au mikono kama saratani
za aina mbalimbali, kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu(blood clot) na
kadhalika.
• Kwa wale wenye kuvimba korodani, ni muhimu kwa daktari
kuchukua kipimo kwa kukwangua sehemu husika kasha kuchanganya na potassium
hydroxide na kutazama kwenye hadubini kama kuna dalili (Meddler bodies, sclerotic
bodies) za ugonjwa wa fangasi unaojulikana kama chromobalstomycosis
(unaosababishwa na fangasi aina ya Fonsecaea pedrosoi, Phialophora verrucosa,
Cladosporium carrionii, au Fonsecaea compacta). Pia ukungu huu huweza kuoteshwa
maabara ili kuangalia kama kuna fangasi aina yoyote ile niliyotaja hapo juu
watakaota.
Tiba ya ugonjwa wa
matende ni nini?
Tiba ya ugonjwa wa
matende hutegemea na sehemu husika. Kwa wagonjwa walio katika jangwa la sahara,
tiba ni dawa aina ya albendazole pamoja na ivermectin. Kwa wagonjwa waliopo
sehemu nyingine duniani tiba huusisha matumizi ya albendazole pamoja
nadiethylcarbamazine. Kusafisha sehemu iliyoathiriwa na ugonjwa wa matende mara
kwa mara husaidia kupunguza dalili na viashiria vya ugonjwa huu.
Kwa wale waliovimba korodani kutokana na ugonjwa wa matende, tiba yake ni upasuaji. Wakati mwingine, kama
mgonjwa atakuwa amevimba sana korodani, basi baada ya kufanyiwa upasuaji wa
kawaida, atahitaji kufanyiwa upasuaji kurekebishwa ngozi yake (plastic
surgery).
Katika utafiti uliofanywa na chuo cha Liverpool school of
tropical medicine mwaka 2005, umeonyesha dawa ya antibiotiki hususan doxycyline
inaweza kutumika kutibu ugonjwa huu wa matende kutokana na minyoo (adult worms)
kuwa na bakteria aina ya wolbachia wanaoishi ndani ya minyoo hii, hivyo dawa
hii hutibu kwa kuua bacteria hawa na kusababisha minyoo hii kufa, na kuondosha
kabisa microfilariae kwenye damu ya mgonjwa na hivyo mgonjwa kupona.
Dawa hii hutumika kwa muda wa wiki 8. Hata hivyo, kama
mgonjwa atakuwa na mabuu ndani ya mfumo wake wa limfu, basi itakuwa vigumu
kwake kupona. Utafiti zaidi unahitajika ili kuwa na uhakika zaidi juu ya dawa
hii kutibu ugonjwa huu.
Kinga ya ugonjwa wa matende ni nini?
• Shirika la afya duniani (WHO) limeanzisha jitihada za
kutokomeza ugonjwa huu wa matende ifikapo mwaka 2020.
• Matumizi ya dawa aina ya albendazole kwa wale walio katika
hatari kupata ugonjwa wa matende unaosababishwa na vimelea.
• Kuvaa viatu wakati wa kutembea nje ili kujikinga kupata
maambukizi ya aina ya podoconiosis.
• Kuosha miguu na mikono kwa kutumia maji na sabuni
• Kuosha miguu kila siku kwa kutumia antiseptic
(bleach).
Comments
Post a Comment